Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania Bara

IJUE SAYANSI YA MOTO NA JINSI YA KUKABILIANA NAO

Matukio ya moto yameendelea kutishia usalama wa Taifa kwa kuteketeza maisha ya watanzania na mali zao kwa ujumla, utafiti unaonesha sababu za matukio hayo ni wananchi kutokuwa na uelewa au kukosa elimu ya moto na wengine  kutozingatia kinga na tahadhari ya majanga ya moto japo wanao uelewa mdogo kuhusu moto.

Kuna vyanzo vingi vya moto  lakini chanzo kikubwa ni  sisi  Binadamu  kwa sababu  ya asili na harakati za maisha ya kila siku,  kuhusisha matumizi ya moto kwa   maana ya mwako,  nishati ya umeme pamoja na vyombo vya usafiri na usafirishaji.  Katika mahitaji hayo inatulazimu kujenga urafiki na moto bila kujali hatari iliyopo.

Aina ubishi kwamba moto ni nyenzo muhimu katika maisha yetu ya kila siku, pia ni adui yetu mkubwa sana anaye penda kutushambulia akitokea ndani ya jengo au chombo cha moto.  Kutokana na hilo , moto  umekuwa ukisababisha  uharibifu wa mali, ulemavu,  pamoja na vifo vya watu kila siku iendayo kwa Mungu.

Hatuwezi kuepuka isitokee kabisa lakini tunaweza kupunguza matukio hayo kama tutapata elimu sahihi ya kinga na taadhali ya majanga ya moto. Mwako au moto ni kitu cha kawaida ambacho mtu yeyote anaweza kutafsiri kwa namna yake lakini kitaalamu.

Moto/Mwako ni mgongano endelevu wa kikemikali ambao uzaa joto na mwanga.  Mgongano  huo  endelevu   utasababisha muwako  ambao  utaendelea   kukua  endapo  utapata  vitu  vitatu vyenye uwiano  ambavyo  ni joto,  hewa  ya  oksijeni  na kuni (vitu  vinavyoungua).

Vitu vinavyoungua vimegawanyika katika mada kuu tatu ambazo ni vitu vigumu, vimiminika na gesi. Vitu hivyo ili viungue vinatakiwa kubadilika katika hali yake ya kawaida na kuwa mvuke (vapor), kati ya vitu hivyo gesi tayari imesha kuwa katika hali ya mvuke hivyo haihitaji kubadilika na ndio maana gesi uwaka kwa hara sana na usambaa kwa muda mfupi pindi janga la moto linapotokea.

Muunganiko wa vitu hivi kwa pamoja huzaa joto na mwanga ambavyo ndio moto. Kisayansi bila ya vitu hivyo moto hauwezi kutokea kwa sababu ni viungo muhimu katika numara sorgulama kuzalisha moto.

Kuwepo kwa visababisha moto kwa pamoja, kunatengeneza pembe tatu za moto, lakini pia kuwepo kwa viungua, joto na oxygen haitoshi kusababisha moto, bali joto hilo lazima liwe juu kuliko joto la kitu kilichopo eneo husika. Joto kazi yake ni kuhakikisha kitu kinachoungua kina badilika na kuwa mvuke, udogo wa kitu utahitaji joto kidogo ukilinganisha na kitu kikubwa.

Mchakato huo ukiungana na hewa ya oxygen isiyopungua asilimia 14% na isiyozidi 21%, Oxygen si miongoni mwa vitu vinavyoungua, bali inasaidia moto kuwaka kwa sababu mara zote moto unahitaji hewa safi.

Utafiti wa kisayansi ulibaini kwamba moto una madaraja manne, ambayo ni daraja “A”, “B”, “C”, “D”, madaraja haya husaidia katika kupambana na majanga ya moto kwa kufahamu mapema kuwa hili ni daraja gani na kizimio chake ni kipi.

Vitu vinavyoungua vyenye asili ya mimea kama mbao, nguo za pamba pamoja na nafaka vilimepewa Daraja “A”.  Moto huu kizimio chake huwa ni maji ambayo kazi yake ni kushusha (kupoza) kiwango cha joto kilichozalishwa na mchanganyiko wa vitu vilivyopo, pamoja na maji pia waweza kutumia kizimia moto cha maji na povu lenye dawa (foam). Unapozima moto kwa kutumia maji hakikisha eneo hilo hakuna umeme kwani maji tukumbuke yanapitisha umeme na unaweza kudhurika.

Daraja lingine la moto ni daraja “B”. Huu ni moto utokanao na vimiminika vinavyoungua ambavyo ni vitu vyenye asili ya mafuta na kizimio chake ni mchanganyiko wa numaradan isim sorgulama maji na povu lenye dawa.

Kazi ya povu ni kufunika vitu vinavyoungua na kuvinyima hewa ya oxygen na wakati huo huo maji yanafanya kazi ya kupoza kiwango cha joto na kushusha kiwango cha oxygen hadi chini ya asilimia 14% hatimaye kusababisha moto uzimike.

Katika daraja “B” la moto kamwe hakikisha hautumii maji kwani maji ni mazito kuliko vimiminika vinavyowaka hivyo upelekea maji kuzama na mafuta kuendelea kubakia juu.

Moto Daraja “C” ni moto wa gesi na vitu vyenye asili hiyo na moto wa daraja hili ni hatari sana. Moto huu kwa kawaida unashambulia kwa haraka sana kwa sababu usambaaji wake ni  wa kasi kubwa kama jinsi gesi inavyosambaa kwenye mzunguko wa hewa.

Jinsi ya kukabiliana nao, ni kufunga au kuziba sehemu inayovujisha gesi, ili kuunyima chakula na kasi yake itapungua.  Kisha tumia kizimio cha unga mkavu wa kemikali (Dry chemical powder) na anza kuuzima kama kuna vitu vingine vinavyoungua.

Kizimio cha hewa mkaa (Carbon dioxide) kitafanya kazi kama tukio hilo limetokea ndani kwa sababu hewa hii ni nyepesi kuliko oxygen, hali inayosababisha iondolewe katika mzunguko na uzimaji wake kuwa mgumu.

Daraja lingine ni “D” ambalo viungua vyake ni madini na vitu vyenye asili ya chuma. Kizimio chake ni mchanga mkavu na unga mkavu (Dry Powder) tukumbuke kuwa chuma ukimwagia maji wakati kinaungua kitapoteza umbo lake la asili hivyo hauruhusiwi kutumia maji.

Pamoja na madaraja hayo, vipo vyanzo vinavyotaja madaraja ya moto kuwa sita kwa kuongeza daraja “E” na “F”. Vyanzo hivi vinasema daraja “E” ni moto wa umeme, lakini kisayansi hakuna moto wa umeme kwani, umeme ni chanzo tu na baada ya kuzima mfumo wake moto utapewa daraja kutokana na vitu vinavyoungua ambavyo lazima vitaingia katika madaraja “A”, “B”, “C” au “D”.

Vyanzo hivyo vinataja daraja “F” kuwa ni moto unaotokana na mafuta mazito ya kula kwa sababu hayalipuki mpaka yachemke. Kwa kuwa tabia na uzito wake (density) pamoja na mbinu za uzimaji wake ni zile zinazotumika katika vimiminika vingine, na kwa kuwa daraja la moto linatokana na vitu vinavyoungua, moto huu unabaki katika daraja “B”.

Kabla hujakabiliana na janga la moto, kwanza hakikisha unazima umeme kama jengo au eneo hilo lina umeme, hatua ya pili ni kutoa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kupiga simu  ya dharura namba 114, toa maelezo kwa ufasaha nini kimetokea, wapi na jinsi gani Jeshi hilo linaweza kufika kwa haraka.

Hatua ya tatu piga kelele kujulisha watu walioko ndani ya jengo na maeneo jirani, toka nje ya jengo elekea eneo la wazi, saidia wagonjwa, walemavu, watoto wazee na wageni kutokanao nje ya jengo.

Kwa kufahamu maana ya moto, madaraja yake na namna ya kukabiliananao, ni dhahiri mtu yeyote atakuwa na uwezo wa kujikinga na majanga ya moto au kupunguza kwa kiwango kikubwa madhara yake pindi yanapotokea.

Changamoto iliyopo hapa kwa baadhi ya wakazi wa maeneo mbalimbali, ni hulka ya kutotilia maanani njia sahihi za tahadhari na namna ya kujikinga na majanga ya moto, na namna ya kutoa ushirikiano wa dhati kwa Jeshi la zimamoto na Uokoaji wakati majanga hayo yanapotokea au kutoa taarifa zisizo za kweli kuhusu matukio ya moto.

Kwa mantiki hiyo, ni jukumu la kila mmoja wetu kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kupata elimu ya moto na kuizingatia kwa lengo la kupunguza au kuondoa kabisa majanga hayo ambayo yanaleta athari kubwa kwa jamii.