Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania Bara

Uncategorized

Msemaji Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkaguzi (INSP) Joseph Mwasabeja (kulia) akisalimiana na Meneja wa Kampuni ya Global Group Bw. Abdallah Mrisho (kushoto) alipotembelea Kampuni hiyo mapema leo.

Mwandishi na Mhariri wa gazeti la amani wa Kampuni ya Global Group Bw. Erick Evalist (kushoto), akitoa ufafanuzi kwa Msemaji Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkaguzi (INSP) Joseph Mwasabeja (wa pili kulia), jinsi Kampuni ya Global Group inavyoendesha shughuli zake kupitia vyombo mbalimbali vilivyopo chini ya kampuni hiyo wakati wa ziara yake yakukuza mahusiano mapema leo.

Msemaji Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkaguzi Joseph Mwasabeja (INSP) (wa pili kulia) akimsikiliza kwa makini mmoja ya watayarishaji wa vipindi wa Kampuni ya Global Group (aliyevaa shati ya blue) wakati wa ziara yake yakukuza mahusiano  alipo tembelea kampuni hiyo mapema leo. (Picha na Jeshi la Zimamoto Na Uokoaji)

IMEANDALIWA NA KITENGO CHA HABARI NA ELIMU KWA UMMA – JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI

Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CF) Billy Mwakatage (kushoto), akiwa ameambatana na mwenyeji wake mmiliki wa Yatch Club Bw. Brian Fernandes (kulia), baada ya kuwasili ofisi za Yatch Club kwa ajili ya uzinduzi wa mafunzo ya uzamiaji majini kina kirefu daraja la pili kwa Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Jijini Dar es Salaam. Alipotembelea eneo hilo mapema leo asubuhi.

Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CF) Billy Mwakatage (wa pili kushoto), akiwa na wakufunzi kutoka nchini Ujerumani na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Wakati wa  uzinduzi wa mafunzo ya uzamiaji majini kina kirefu daraja la pili kwa Askari wa Jeshi hilo Jijini Dar es Salaam. Alipotembelea eneo hilo mapema leo asubuhi.

Mkufunzi kutoka nchini Ujerumani Bw. Dan Jungingfer (kulia), akitoa maelekezo ya mbinu za uzamiaji majini kwenye kina kirefu kwa Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Sajini Gift Longwe na Konstebo Baltazari Swai. Wakati wa  uzinduzi wa mafunzo ya uzamiaji majini kina kirefu daraja la pili kwa Askari wa Jeshi hilo Jijini Dar es Salaam. (Picha na Jeshi la Zimamoto Na Uokoaji)

Mafunzo haya yanayoendeshwa hapa nchini na Wakufunzi kutoka Ujerumani yana lengo la kuwaongezea Maafisa na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji weledi katika kukabiliana na majanga ya mafuriko na kuzama kwa watu majini haswa kwenye kina kirefu.

IMEANDALIWA NA KITENGO CHA HABARI NA ELIMU KWA UMMA – JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI

Picha ni sehemu ya bweni lililoathirika na moto na kuteketeza mali za Wanafunzi. (Picha na Maktaba)

Jeshi la  Zimamoto na Uokoaji ndicho chombo chenye jukumu la kuzuia na kukabiliana na majanga  mbalimbali   kama mafuriko , Tetemeko la  Ardhi,  ajali  za vyombo vya usafiri na usafirishaji,  kuporomoka kwa majengo, migodi,  pamoja na matukio ya moto. 

Mara kwa mara, majanga ya moto yamekuwa yakitokea katika jamii yetu kwa sababu moto ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku.  Utafiti umethibitisha  kwamba,  vyanzo vingi vya moto ni sisi wenyewe (binadamu)  kutokana na uzembe,   hujuma  au kutokukuwa na  elimu ya Tahadhali na Kinga  Dhidi ya  Moto.

Aidha, matukio ya moto yamekuwa  yakitokea mara kwa mara katika shule za bweni hapa nchini  hususani shule za sekondari,  na kusababisha  uharibifu wa miundo mbinu kama vile Mali, majengo na wakati mwingine majeraha au vifo kwa wanafunzi wetu na kuleta simanzi na sintofahamu kwa Wananchi na Taifa kwa ujumla .

Uchunguzi  wa moto (Fire Investigation)  umebaini     sababu  za matukio hayo ni matumizi mabaya ya umeme yanayofanywa na   wanafunzi  kwa  kujiunganishia nyaya za umeme wenyewe bila kuwa na weledi iliwapate  sehemu za kuchaji simu na heater za kuchemshia maji kwa kificho kwa sababu Wanafunzi  hawaruhusiwi kuwa na simu wala heater pindi wanapokuwa shuleni.

Lakini pia sababu nyingine ni matumizi ya mishumaa, unapokatika umeme wakati wa kujisomea. Shule nyingi  zinajaribu kuzuia mabweni kutumika kama sehemu za kujisomea,  lakini  bado wapo baadhi ya Wanafunzi  wanaamua   kujisomea  ndani ya  mabweni  bila kuchukua  tahadhari yoyote na wanapopitiwa na usingizi,  uacha mishumaa inaendelea kuwaka na hatimaye kusababisha ajali ya moto.

Utakumbuka miaka kadhaa iliyopita matukio kama haya ya kuungua kwa shule yalileta majonzi  makubwa kwa kuangamiza  maisha ya Wanafunzi wengi.  Kuungua kwa shule ya Shauritanga Mkoani Kilimanjaro mwaka 1994 ambapo zaidi ya wanafunzi 40 walipoteza Maisha pamoja na Mali.

Mwaka 2009 shule ya sekondari Idodi Mkoani Iringa iliteketea kwa moto na zaidi ya wanafunzi 20 walipoteza Maisha pamoja na Mali. Hiyo ni mifano tu lakini matukio ya kuungua kwa shule ni mengi sana hapa nchini.

Ili kupunguza matukio hayo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeanzisha Fire klabu  katika shule mbalimbali  za Msingi na Sekondari ili kupata wajumbe  watakaoliwakilisha  katika shule na makazi yao.

Kwa kutumia fire klabu, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji  limejenga ukaribu mkubwa na Wanafunzi wa shule hizo,  hatua inayosaidia kuwapa elimu stahiki ya kukabiliana na majanga ya moto.

Changamoto  iliyopo ni  mapokeo ya baadhi ya Viongozi wa shule kutokuwa tayari kuruhusu shule zao kuanzisha  klabu za Zimamoto zinazosimamiwa na  kuratibiwa na Jeshi hilo ambapo mpaka sasa ni shule 100 ndizo zilizofungua klabu hizo kwa nchi nzima.

Kama nilivyo eleza hapo mwanzo, lengo la klabu hizo ni kuwapa fursa wanafunzi kuwa familia moja na wataalamu wa Zimamoto. Ukaribu huo hutumika kwa wazimamoto kuwapa mbinu mbalimbali za kuzuia na kukabiliana na vyanzo vya moto.

Lakini  kwa upande wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,  ni kupanua wigo wa kuwa na idadi kubwa ya  watu, wanaoifahamu vyema  elimu  hiyo  na kuwa  mabalozi  wazuri  watakao liunganisha Jeshi  na jamii kwa kufikisha  elimu hiyo, Mijini  na Vijijini na hatimaye kuweza kupunguza na kutokomeza kabisa majanga.

Wito wangu kwa wamiliki wa shule, walipokee jambo hili kama ukombozi kwao kupunguza majanga  ya moto katika shule zao.

Tukishirikiana tutapunguza majanga ya moto, na Taifa litakuwa salama.

Mungu ibariki Afrika Mungu ibariki Tanzania.

IMEANDALIWA NA KITENGO CHA HABARI NA ELIMU KWA UMMA – JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI

Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CF) Billy Mwakatage, akiwapa pole Waathirika wa moto ulioteketeza vibanda vya Wafanyabiashara wa Soko la Nguo Mbagala Temeke Jijini Dar es Salaam. Alipotembelea eneo hilo mapema leo asubuhi.

Kamaishna wa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CF) Billy Mwakatage akimfariji kwa kumpa pole Mama lishe Bi. Fatma Hassan aliyeunguliwa na vitendea kazi vyake kufuatia tukio la kuungua kwa moto kwa soko la nguo Mbagala.  Alipotembelea eneo hilo mapema leo asubuhi.

Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CF) Billy Mwakatage (kulia) akikagua eneo la Soko la Nguo Mbagala lililoteketea kwa moto juzi. Alipotembelea eneo hilo mapema leo asubuhi. (kushoto) ni Mwenyekiti Msaidizi wa Wafanyabiashara Harruni Kwemeye.

Sehemu ya Wafanyabiashara wa Soko la Nguo Mbagala Temeke Jijini Dar es Salaam walioathirika na moto ulioteketeza vibanda vya wafanyabiashara hao juzi. (Picha na Jeshi la Zimamoto Na Uokoaji)

Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini (CGF), Thobias Andengenye amewapandisha vyeo Askari wawili (2) wa Jeshi hilo kutokana na utendaji uliotukuka. Kamishna Jenerali amewapandisha vyeo kwa Mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa sheria.

CGF Thobias Andengenye, amefanya hivyo kutimiza Mamlaka hiyo ambayo ipo kwa mujibu wa sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Na. 14 ya mwaka 2007 na Kanuni ya Utumishi ya Jeshi hilo ya mwaka 2008.

Katika zoezi hilo amewapandisha vyeo Askari kutoka Konstebo wa Zimamoto kuwa Sajini wa Zimamoto, Askari waliopandishwa vyeo ni Konstebo Aloyce Zengwe ambaye alishiriki matembezi ya Skauti kwa kupeperusha bendera ya Jeshi hilo kutoka Morogoro mpaka Dodoma huku akihamasisha Wananchi kushirikiana na Jeshi hilo katika swala zima la Kuokoa Maisha na Mali.

Mwingine ni Konstebo Bahati Lugodisha aliyeshiriki Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2017. Aidha Kamishna Jenerali aliwapa pongezi Askari waliopanda vyeo ambao hakika wanastahili na kuwataka watumie vyeo hivyo vipya kutimiza majukumu yao kwa weledi.

Akitangaza kupitia Force Order Na.FRF 09/2018 ya tarehe 02 March, 2018. Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji amewapongeza NCO hao kwa kupanda vyeo. “Hakika wanastahili na nawatakia utendaji mwema” alisema Kamisha Jenerali.

IMEANDALIWA NA KITENGO CHA HABARI NA ELIMU KWA UMMA – JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI

 

 

Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini (CGF), Thobias Andengenye amewapandisha vyeo askari 283 katika Mikoa yote Tanzania Bara. Kamishna Jenerali amewapandisha vyeo leo kwa Mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa sheria.

Kamishna Jenerali (CGF) Thobias Andengenye, amefanya hivyo kutimiza mamlaka hiyo ambayo ipo kwa mujibu wa sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Na. 14 ya 2007 na Kanuni ya Utumishi ya Jeshi hilo ya mwaka 2008.

Katika zoezi hilo amewapandisha vyeo Askari kutoka Sajini kuwa Stesheni Sajini 43, wengine 129 kutoka Koplo kuwa Sajini pamoja na 111 kutoka Konstebo kuwa Koplo na kuwataka Askari hao kufanya kazi kwa bidii.

“Mliopanda vyeo leo sio kwamba ninyi ni bora zaidi ya wengine bali ni kwa sababu ya bidii yenu kazini” alisema Kamishna Jenerali. Pia ni vema ambao hamjabahatika kupenda vyeo leo muongeze bidii katika utendaji kazi wenu.

Aidha Kamishna Jenerali aliwapa pongezi Askari waliopanda vyeo ambao hakika wanastahili na kuwataka watumie vyeo hivyo vipya kutimiza majukumu yao kwa weledi.

Naye Stesheni Sajini Ignas Uria amemshukuru Kamishna Jenerali na ameahidi kuongeza juhudi katika kukitumikia cheo hicho kwa weledi zaidi, huku akiwataka Askari wachini ya cheo chake na wajuu kushirikiana kwa pamoja katika kulitumikia Jeshi na Taifa kwa Ujumla.

IMEANDALIWA NA KITENGO CHA HABARI NA ELIMU KWA UMMA – JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI

Mkuu wa Kitengo cha Uchumi na Takwimu Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (ACF) Maria Kullaya amepokea msaada wa Kompyuta mpakato moja na Printa moja kutoka katika Kampuni ya Tanzania Tooku Garment Co.Ltd, kwa ajili ya kuboresha kitengo cha Takwimu cha Jeshi hilo.

Msaada huo wenye thamani ya sh.1.5 million ambao umetolewa na Kampuni ya Tanzania Tooku Garment Co.Ltd umepokelewa mapema leo Makao Makuu ya Jeshi hilo yaliopo barabara ya Ohio Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati akipokea msaada huo Kamishna Msaidizi Maria alisema, msaada huu umetolewa wakati muafaka kwani utasaidia kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi katika ukusanyaji wa taarifa na utunzaji wa kumbukumbu tofauti na hapo awali.

Tunatarajia kuvitumia vifaa hivi kwa lengo mahususi pamoja na kuvitunza vizuri “Vifaa hivi vitakuwa chachu kwa kitengo cha takwimu kwani tulikuwa na uhaba wa vitendea kazi” alisema Kamishna Msaidizi Maria.

Naye Meneja wa Kampuni hiyo Bw. Rigobert Massawe, akizungumza wakati akikabidhi msaada huo, alisema “lengo ni kuliwezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kutimiza majukumu yake kwa ufanisi kwani kwa kufanya hivyo tunatimiza wajibu wetu wa kurudisha huduma kwa jamii”.

Kamishna Msaidizi Maria anaishukuru kampuni hiyo kwa kuwapa msaada wa vitendea kazi hivyo, pia kupitia nafasi hii naomba wadau wengine waige mfano huu kwa kulisaidia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Nyanja mbalimbali ili liweze kutimiza majukumu yake ya kuokoa Maisha na Mali za Watanzania.

Mkuu wa Kitengo cha Uchumi na Takwimu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Kamishna Msaidizi (ACF) Maria Kullaya (kulia) akipokea msaada wa Kompyuta mpakato na Printa kutoka kwa Meneja wa Kampuni ya Tanzania Tooku Garment Co.ltd Bw. Rigobert Massawe (kushoto). Vifaa vitakavyosaidia kutunza kumbukumbu za takwimu za majanga mbalimbali yanayotokea nchini, msaada huo umepokelewa Makao Makuu ya Jeshi hilo mapema leo.

Mkuu wa Kitengo cha Uchumi na Takwimu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Kamishna Msaidizi (ACF) Maria Kullaya wa nne kutoka (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Meneja wa Kampuni ya Tanzania Tooku Garment Co.ltd Bw. Rigobert Massawe wa tano kutoka (kulia), Meneja rasilimali watu wa Kampuni hiyo Bw. Danial Mbonea wa tatu kutoka (kulia) na Maafisa wa Jeshi hilo wakati wa makabidhiano ya msaada wa Komputa mpakato na Printa, mapema leo Makao Makuu ya Jeshi hilo.

Meneja wa Kampuni ya Tanzania Tooku Garment Co.ltd Bw. Rigobert Massawe (kushoto) akimkabidhi Kompyuta mpakato (Laptop) Mkuu wa Kitengo cha Uchumi na Takwimu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Kamishna Msaidizi (ACF) Maria Kullaya (kulia) (Picha na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji)

IMEANDALIWA NA KITENGO CHA HABARI NA ELIMU KWA UMMA – JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI

Leave a comment  1