Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini (CGF), Thobias Andengenye amewapandisha vyeo Askari wawili (2) wa Jeshi hilo kutokana na utendaji uliotukuka. Kamishna Jenerali amewapandisha vyeo kwa Mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa sheria.

CGF Thobias Andengenye, amefanya hivyo kutimiza Mamlaka hiyo ambayo ipo kwa mujibu wa sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Na. 14 ya mwaka 2007 na Kanuni ya Utumishi ya Jeshi hilo ya mwaka 2008.

Katika zoezi hilo amewapandisha vyeo Askari kutoka Konstebo wa Zimamoto kuwa Sajini wa Zimamoto, Askari waliopandishwa vyeo ni Konstebo Aloyce Zengwe ambaye alishiriki matembezi ya Skauti kwa kupeperusha bendera ya Jeshi hilo kutoka Morogoro mpaka Dodoma huku akihamasisha Wananchi kushirikiana na Jeshi hilo katika swala zima la Kuokoa Maisha na Mali.

Mwingine ni Konstebo Bahati Lugodisha aliyeshiriki Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2017. Aidha Kamishna Jenerali aliwapa pongezi Askari waliopanda vyeo ambao hakika wanastahili na kuwataka watumie vyeo hivyo vipya kutimiza majukumu yao kwa weledi.

Akitangaza kupitia Force Order Na.FRF 09/2018 ya tarehe 02 March, 2018. Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji amewapongeza NCO hao kwa kupanda vyeo. “Hakika wanastahili na nawatakia utendaji mwema” alisema Kamisha Jenerali.

IMEANDALIWA NA KITENGO CHA HABARI NA ELIMU KWA UMMA – JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI

 

 

Share this post on: