Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini (CGF), Thobias Andengenye amewapandisha vyeo askari 283 katika Mikoa yote Tanzania Bara. Kamishna Jenerali amewapandisha vyeo leo kwa Mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa sheria.

Kamishna Jenerali (CGF) Thobias Andengenye, amefanya hivyo kutimiza mamlaka hiyo ambayo ipo kwa mujibu wa sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Na. 14 ya 2007 na Kanuni ya Utumishi ya Jeshi hilo ya mwaka 2008.

Katika zoezi hilo amewapandisha vyeo Askari kutoka Sajini kuwa Stesheni Sajini 43, wengine 129 kutoka Koplo kuwa Sajini pamoja na 111 kutoka Konstebo kuwa Koplo na kuwataka Askari hao kufanya kazi kwa bidii.

“Mliopanda vyeo leo sio kwamba ninyi ni bora zaidi ya wengine bali ni kwa sababu ya bidii yenu kazini” alisema Kamishna Jenerali. Pia ni vema ambao hamjabahatika kupenda vyeo leo muongeze bidii katika utendaji kazi wenu.

Aidha Kamishna Jenerali aliwapa pongezi Askari waliopanda vyeo ambao hakika wanastahili na kuwataka watumie vyeo hivyo vipya kutimiza majukumu yao kwa weledi.

Naye Stesheni Sajini Ignas Uria amemshukuru Kamishna Jenerali na ameahidi kuongeza juhudi katika kukitumikia cheo hicho kwa weledi zaidi, huku akiwataka Askari wachini ya cheo chake na wajuu kushirikiana kwa pamoja katika kulitumikia Jeshi na Taifa kwa Ujumla.

IMEANDALIWA NA KITENGO CHA HABARI NA ELIMU KWA UMMA – JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI

Share this post on: